Friday, September 18, 2009

DAR ES SALAAM,

Bwana Madaraka Nyerere ambaye ni mtoto wa rais wa zamani Tanzania Hayati Mwl. Julius Nyerere pamoja na Jaffar Amini ambaye ni mtoto wa raisi wa zamani wa Uganda Iddi Amin kwa pamoja wanatarajia kupanda mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kuchangisha fedha za hisani kuwasaidia watoto yatima wanaolelewa na asasi isiyo ya kiserikali ya Community Alive iliyoko mjini Musoma.

Akizungumza na waandishi wa habari leo kwenye Ukumbi wa Idara ya habari Maelezo Bwana Madaraka Nyerere amesema hatua hiyo pia inalenga kumuenzi baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambapo kwa pamoja wanatarajia kuanza kupanda mlima huo Octoba 29 hadi Novemba 6 mwaka huu.

Bwana Madaraka amewaomba wananchi mbalimbali kuchangia asasi hiyo ili kufanikisha lengo lake la kuwasaidia watoto hao ambao wameachwa na wazazi wao kutokana na ugonjwa wa Ukimwi kupitia namba ya akaunti 064-6000246 kwenye benki ya Barclays tawi la Musoma kupitia jina la Community Alive.

Hii ni mara ya pili kwa Bwana Madaraka kuchangisha fedha za hisani ambapo mwaka jana alifanikiwa kuchagisha kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 22 zilizowezesha ujenzi wa mabweni ya shule ya Sekondari ya wasichana ya Mtemi Edward Wanzagi iliyopo mkoani Mara.

Hayati Mwalimu Nyerere na Iddi Amini walikuwa na tofauti kubwa za kisiasa kitu kilichopelekea kuvunjika kwa iliyokuwa jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977 na chanzo cha vita vya Kagera mwaka 1979.

No comments:

Post a Comment