Thursday, October 22, 2009

MTOTO AFA KWA KUKEKETWA

Na Jamillah wa MAJIRA
POLISI Mkoani Manyara wanamshikilia Bw.Danieli Shauri(37)kwa kosa la kumkeketa binti yake,Debora Daniel (4) na kumsababishia kifo.
Mtoto huyo alikeketwa oktoba 11,mwaka huu na kuendelea kuvuja damu sehemu za siri hadi oktoba 18 alipofariki dunia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa manyara,Parmena Sumary alisema kuwa tukio hilo limetokea siku hiyo saa 10.00 jioni katika kijiji cha Imbilili Wilayani Babati.
Kamanda Sumary alisema kabla ya kifo chake,mtoto huyo alikuwa akiishi na mtuhumiwa baada ya mama yake mzazi,Bi.Catherine Daniel(29)kupata kichaa na kumtelekeza akiwa mdogo.
Kutokana na hali hiyo mtoto alikosa afya na kupata homa za marakwa mara kwasababu ya kukosa maziwa ya mama,hali iliyosababisha wazazi wa mtuhumiwa kushauri akeketwe ili kuondokana na matatizo hayo.
Kamanda alisema kuwa mtuhumiwa alitekeleza ushauri potofu wa wazazi wake,lakini alishangazwa na hali ya mtoto huyo kuendelea kuwa mbaya hadi alipofariki dunia kwa kupoteza damu nyingi.
Baada ya kifo hichokutokea,mtuhumiwa alitaka kuuzika mwili wa mtoto huyo bila ya watu kujua lakini wasamaria walitoa taarifa kwa mtendaji wa kijiji hicho,Patizimu Joseph ambaye alifika nyumbani kwa mtuhumiwa na kukuta maandalizi ya mazishi na kuwaamuru kusimamisha shughuli hiyo hadi hatua za kisheria zitakapofuatwa
Baada ya amri hiyo mwili huo ulichukuliwa hadi hospitali ya wilwya ya Babati kwa uchunguzi zaidi na ndipo iligundulika kuwa marehem alipatwa na mauti hayo baada ya kukeketwa na kuvuja damu nyingi.
Kwa mujibu wa kamanda huyo,ngariba aliyehusika kumkeketa mtoto huyo,Mama Mangiza,alitoroka baada ya hali ya mtoto na polisi wanaendelea kumsaka kujibu shtaka hilo.

No comments:

Post a Comment