Wednesday, December 15, 2010

NJAA YASUMBUA WAKAZI WAKATA YA NDULI MKOANI IRINGA.

NJAA YASUMBUA WAKAZI WAKATA YA NDULI MKOANI IRINGA.
WALIHAIDIWA KUPEWA CHAKULA CHA
MSAADA NA WAGOMBEA WAO.

Wananchi wa kata mpya ya Nduli katika Manispaa ya Iringa wameomba kupatiwa chakula cha msaada kutokana na njaa kali inayowakabili kwa madai kuwa tangu waiombe serikali iwapatie msaada huo, hawajawahi kusaidiwa.

Imedaiwa kuwa Wananchi hao wamekuwa wakila mlo mmoja kwa siku na wanafunzi wa shule za msingi wameathirika zaidi kwa kuwa shule nyingi hazina uwezo wa kuwaandalia wanafunzi chakula cha mchana hali inayopelekea kutokuwa na isikivu wa kutosha wanapokuwa darasani.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nduli, Ayubu Mwenda alisema tatizo la chakula limekuwa kubwa, kutokana na mazao mengi kukauka kabla ya kukomaa kufuatia ukame ulioathiri kata yao.

Amesema tatizo hilo, limeshusha kwa kiasi kikubwa kiwango cha wanafunzi kufaulu kwa madai kuwa wengi wao wamekuwa wakienda shule bila kula chochote hadi jioni wanaporejea nyumbani.

Wananachi hao walisema kuwa wakati wa kampeni, waliahidiwa kupewa chakula na wagombea wao, lakini bado hawajakumbukwa jambo ambalo linawafanya waanze kukosa imani na viongozi waliowaweka madarakani.

Kwa upande wake diwani mpya wa Kata ya Nduli, aliahidi kutoa chakula cha msaada kwa ajili ya wanafunzi wa maeneo ya kata hiyo mara shule itakapofunguliwa na kwamba hivi sasa hawezi kutokana na ukweli kwamba bado hawajaanza kazi.

Takwimu za awali zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa wakati kata hiyo haijahamishiwa katika Halmshauri ya Manispaa, zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 13,000 wanakabiliwa na tatizo la njaa katika kata hiyo.

Monday, December 6, 2010

MATOKEO YA MITIHANI DARASA LA SABA YATANGAZWA

Na.Joyce Mtavangu.
Njombe
Imeelezwa kuwa hali ya utoro ambayo imekithiri miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi ndio chanzo cha kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi wanao hitimu darasa la saba katika wilaya ya njombe mkoani Iringa.

Hayo yamesemwa na afisa elimu wilaya ya njombe Bw Bartazar Kessy. alipokuwa akizungumza Ofisini kwake ambapo amesema kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kimeshuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo upungufu wa walimu,ukilinganisha na msongamano pamoja na utoro.

Aidha katika kupambana na adha ya kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi hao, Serikali imeweka mkakati wa kutoa vyakula mashuleni ili kukabiliana na tatizo la utoro ambalo ndiyo chanzo cha wanafunzi wengi kufeli.Hata hivyo ameongeza kuwa ufaulu kwa mwaka huu umeshuka kwa asilimia 0.29 ukilinganisha na mwaka jana ambapo kiwango cha kufaulu kilikuwa ni asilimia 66.27 tofauti na mwaka huu ambapo kiwango cha wanafunzi waliofaulu ni asilimia 65.5.

Pia bwana Kessy amesema idadi ya wanafunzi waliofanya mtihani ni 9100 kwa wilaya nzima,ambapo idadi ya waliojiandikisha ni 9210,huku waliofaulu ni 5969.Bwana Kessy amewataka wazazi kutoa ushirikiano kwa walimu ikiwa ni pamoja na kufuatilia mwenendo wa taaluma na kusaidiana na kamati ya shule kuimarisha mazingira ya shule.

Friday, December 3, 2010

WANAFUNZI WAFA KWA AJALI

Na John Gagarini, Kibaha

WANAFUNZI wawili wa sekondari wamekufa na watu wengine wanne kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kugonga mnazi.Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Absalom Mwakyoma alisema kuwa ajali hiyo ilitokea
Desemba Mosi mwaka huu majira ya saa 1:45 usiku katika Kijiji cha Kiguza barabara ya Kilwa wilayani Mkuranga.Kamanda Mwakyoma alisema kuwa gari hilo lenye namba za usajili T 608 APK aina ya Toyota Hilux lilikuwa likiendeshwa na Bi. Anna Kangidaly (56) mkazi wa Tegeta Jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa gari hilo ambalo haikufahamika lilikuwa linatoka wapi liliacha njia na kugonga mnazi na kusababisha vifo vya wanafunzi hao.
Aliwataja wanafunzi waliokufa kuwa ni Aziza Abdallah (15) ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Tinge ambaye alifariki baada ya kufikishwa kwenye hospitali ya
Wilaya ya Mkuranga na Nasoro Mchurubi (15) mwanafunzi wa Shule ya sekondari ya Mguruwe, Kilwa ambaye alifia Hospitali ya Muhimbili.

Aliwataja majeruhi kuwa ni Siyenu Nobileki (16), mwanafunzi wa Sekondari ya Miguruwe, Kilwa, Asia Mohamed (38) mfanyabiashara mkazi wa Kunduchi, Amina Said Kibuli (50) wa Charambe na Maria Ngokoya (55) mkulima mkazi wa Kawe ambao walitibiwa kwenye hospitali ya Mkuranga na kuruhusiwa.

Kamanda Mwakyoma alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika mara moja na dereva anashikiliwa na jeshi hilo kwa uchunguzi zaidi juu ya tukio hilo.

Friday, November 6, 2009

MAPENDEKEZO/USHAURI YA MAREKEBISHO YA SHERIA

MSWADA WA SHERIA YA HAKI YA MTOTO WA 2009(UPANDE WA WAPINZANI)
1)Haki ya kutoa maoni
2)Tafsiri ya mtoto
3)Chombo cha kusimamia sheria n.k

MAPENDEKEZO/USHAURI YA MAREKEBISHO YA SHERIA

MSWADA WA SHERIA YA HAKI YA MTOTO WA 2009(WABUNGE WA KAMATI YA MAENDELEO YA JAMII
1)Tafsiri ya mtoto.
2)Sehem ya kutunzia watoto wadogo iongezwe.
3)Mlezi kumpatia mtoto haki yake ya msingi/mirasi.
4)Serikali itenge sehemu maalumu ya michezo (kucheza watoto).
5)Wazazi,walezi,watoe ushirikiano kwa mtoto aliyepotea.
6)Mahakama za watoto zitengwe mbali na mahakama za watuwazima ili kutoa huoga kwa watoto kujielezea

Wednesday, October 28, 2009

MH.NAGU AZUNGUMZA NA WAZAZI

DAR ES SALAAM,

WAZAZI nchini wanatakiwa kuwazoeza watoto kujenga tabia ya kujisomea vitabu vya ziada na vile vya kiada ili kujenga taifa lenye viongozi wazuri hapo baadae.

Wito huo umetolewa ivi karibuni na Waziri wa Viwanda na Masoko Mary Nagu alipokuwa anafungua tamasha la 18 la Taifa la maonyesho ya vitabu kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza Wilayani Kinondoni.

Waziri Nagu amesema kuwa kasi ya Watanzania katika usomaji wa vitabu bado hauridhishi kutokana na wengi wao kutumia muda mwingi kwenye shughuli nyingine pamoja na starehe hivyo kukosa muda wa kusoma vitabu au kuwahimiza watoto kufanya hivyo.

Hata hivyo Waziri Nagu amekiri kuwa Serikali haijaiwezesha vizuri tasnia ya vitabu nchini ingawa inafanya jitihada za kuandaa mazingira mazuri kwenye tasnia hiyo ili ifanye vizuri.

Tamasha hilo lenye kauli mbiu SOMA VITABU UJIENDELEZE, UJIKOMBOE litaendelea kwa muda wa wiki moja na linajumuisha wadau mbalimbali wa vitabu nchini na nchi nyingine za Afrika Mashariki pamoja na Rwanda.

Thursday, October 22, 2009

MTOTO AFA KWA KUKEKETWA

Na Jamillah wa MAJIRA
POLISI Mkoani Manyara wanamshikilia Bw.Danieli Shauri(37)kwa kosa la kumkeketa binti yake,Debora Daniel (4) na kumsababishia kifo.
Mtoto huyo alikeketwa oktoba 11,mwaka huu na kuendelea kuvuja damu sehemu za siri hadi oktoba 18 alipofariki dunia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa manyara,Parmena Sumary alisema kuwa tukio hilo limetokea siku hiyo saa 10.00 jioni katika kijiji cha Imbilili Wilayani Babati.
Kamanda Sumary alisema kabla ya kifo chake,mtoto huyo alikuwa akiishi na mtuhumiwa baada ya mama yake mzazi,Bi.Catherine Daniel(29)kupata kichaa na kumtelekeza akiwa mdogo.
Kutokana na hali hiyo mtoto alikosa afya na kupata homa za marakwa mara kwasababu ya kukosa maziwa ya mama,hali iliyosababisha wazazi wa mtuhumiwa kushauri akeketwe ili kuondokana na matatizo hayo.
Kamanda alisema kuwa mtuhumiwa alitekeleza ushauri potofu wa wazazi wake,lakini alishangazwa na hali ya mtoto huyo kuendelea kuwa mbaya hadi alipofariki dunia kwa kupoteza damu nyingi.
Baada ya kifo hichokutokea,mtuhumiwa alitaka kuuzika mwili wa mtoto huyo bila ya watu kujua lakini wasamaria walitoa taarifa kwa mtendaji wa kijiji hicho,Patizimu Joseph ambaye alifika nyumbani kwa mtuhumiwa na kukuta maandalizi ya mazishi na kuwaamuru kusimamisha shughuli hiyo hadi hatua za kisheria zitakapofuatwa
Baada ya amri hiyo mwili huo ulichukuliwa hadi hospitali ya wilwya ya Babati kwa uchunguzi zaidi na ndipo iligundulika kuwa marehem alipatwa na mauti hayo baada ya kukeketwa na kuvuja damu nyingi.
Kwa mujibu wa kamanda huyo,ngariba aliyehusika kumkeketa mtoto huyo,Mama Mangiza,alitoroka baada ya hali ya mtoto na polisi wanaendelea kumsaka kujibu shtaka hilo.