Wednesday, October 28, 2009

MH.NAGU AZUNGUMZA NA WAZAZI

DAR ES SALAAM,

WAZAZI nchini wanatakiwa kuwazoeza watoto kujenga tabia ya kujisomea vitabu vya ziada na vile vya kiada ili kujenga taifa lenye viongozi wazuri hapo baadae.

Wito huo umetolewa ivi karibuni na Waziri wa Viwanda na Masoko Mary Nagu alipokuwa anafungua tamasha la 18 la Taifa la maonyesho ya vitabu kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza Wilayani Kinondoni.

Waziri Nagu amesema kuwa kasi ya Watanzania katika usomaji wa vitabu bado hauridhishi kutokana na wengi wao kutumia muda mwingi kwenye shughuli nyingine pamoja na starehe hivyo kukosa muda wa kusoma vitabu au kuwahimiza watoto kufanya hivyo.

Hata hivyo Waziri Nagu amekiri kuwa Serikali haijaiwezesha vizuri tasnia ya vitabu nchini ingawa inafanya jitihada za kuandaa mazingira mazuri kwenye tasnia hiyo ili ifanye vizuri.

Tamasha hilo lenye kauli mbiu SOMA VITABU UJIENDELEZE, UJIKOMBOE litaendelea kwa muda wa wiki moja na linajumuisha wadau mbalimbali wa vitabu nchini na nchi nyingine za Afrika Mashariki pamoja na Rwanda.

Thursday, October 22, 2009

MTOTO AFA KWA KUKEKETWA

Na Jamillah wa MAJIRA
POLISI Mkoani Manyara wanamshikilia Bw.Danieli Shauri(37)kwa kosa la kumkeketa binti yake,Debora Daniel (4) na kumsababishia kifo.
Mtoto huyo alikeketwa oktoba 11,mwaka huu na kuendelea kuvuja damu sehemu za siri hadi oktoba 18 alipofariki dunia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa manyara,Parmena Sumary alisema kuwa tukio hilo limetokea siku hiyo saa 10.00 jioni katika kijiji cha Imbilili Wilayani Babati.
Kamanda Sumary alisema kabla ya kifo chake,mtoto huyo alikuwa akiishi na mtuhumiwa baada ya mama yake mzazi,Bi.Catherine Daniel(29)kupata kichaa na kumtelekeza akiwa mdogo.
Kutokana na hali hiyo mtoto alikosa afya na kupata homa za marakwa mara kwasababu ya kukosa maziwa ya mama,hali iliyosababisha wazazi wa mtuhumiwa kushauri akeketwe ili kuondokana na matatizo hayo.
Kamanda alisema kuwa mtuhumiwa alitekeleza ushauri potofu wa wazazi wake,lakini alishangazwa na hali ya mtoto huyo kuendelea kuwa mbaya hadi alipofariki dunia kwa kupoteza damu nyingi.
Baada ya kifo hichokutokea,mtuhumiwa alitaka kuuzika mwili wa mtoto huyo bila ya watu kujua lakini wasamaria walitoa taarifa kwa mtendaji wa kijiji hicho,Patizimu Joseph ambaye alifika nyumbani kwa mtuhumiwa na kukuta maandalizi ya mazishi na kuwaamuru kusimamisha shughuli hiyo hadi hatua za kisheria zitakapofuatwa
Baada ya amri hiyo mwili huo ulichukuliwa hadi hospitali ya wilwya ya Babati kwa uchunguzi zaidi na ndipo iligundulika kuwa marehem alipatwa na mauti hayo baada ya kukeketwa na kuvuja damu nyingi.
Kwa mujibu wa kamanda huyo,ngariba aliyehusika kumkeketa mtoto huyo,Mama Mangiza,alitoroka baada ya hali ya mtoto na polisi wanaendelea kumsaka kujibu shtaka hilo.

Friday, October 9, 2009

DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Maendeleo ya jamii,jinsia na watoto,Bibi Margareth Sitta,amesema kupitia sheria mpya ya haki ya mtoto,walezi watakaobainika kuwanyanyasa watoto watalipishwa faini kati ya shilingi 500,000 hadi milioni mbili.

Waziri Sitta,amesema sheria hiyo ya mwaka 2009,ndiyo itakayokomesha unyanyasaji wa watoto unaofanywa hivi sasa na baadhi ya walezi nchini ambao umekithiri katika jamii.

waziri Sitta,ametoa kauli hiyo ivi karibuni wakati wa mjadala kuhusu mswada wa sheria hiyo uliohusisha wadau husika kabla ya kuwasilishwa bungeni

Amesema,awali kulikuwa hakuna sheria madhubuti inayolinda haki ya mtoto nchini,lakini kupitia sheria hiyo ana imani kuwa haki hizo sasa zitapatikana ipasavyo na kukomesha unyanyasaji huo

Waziri Sitta,amesema sheria hiyo imeainisha haki zote za mtoto hivyo vituo na walezi wakiwemo mama wakambo watakaokiuka haki hizo watachukuliwa hatua za kisheria.